Makamu wa rais azindua sera ya Taifa ya huduma ndogo za fedha ya mwaka 2017

0

Na Jasmine Shamwepu,Dodoma.

MAKAMU wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania SAMIAH SULUHU HASSAN amezindua sera ya Taifa ya huduma ndogo za fedha ya mwaka 2017 pamoja na mkakati wa utekelezaji wa mwaka 2017/2018 hadi 2027/2028 huku akizitaka taasisi za fedha nchini kuangalia kwa kina suala la riba linalokuwepo kwenye mikopo kwa kuwa limekuwa likiwaumiza wananchi wa hali ya chini.

Akizindua sera hiyo leo mjini Dodoma amesema lengo la kutoa mikopo hiyo ni kuwainua watanzania kiuchumi na sio kuwarudisha nyuma.

Amesema uwepo wa riba kubwa unawarudisha nyuma hasa kwa wafanyabiashara wadogo wadogo na kwamba hali hiyo haipambani na umaskini bali wanapigana na wamaskini au mafukara.

Aidha amewaasa kuwawezesha wanawake sio kiuchumi tu bali kuwapa elimu nyingine kama ya afya ya uzazi,kujua kusoma na ujuzi wa elimu ya biashara.

Amesema uwepo wa sera hiyo ni ushahidi tosha wa dhamira ya dhati ya serikali katika kuimarisha huduma za kifedha nchini na kuwa bora zaidi na kushauri kufanyika kwa tathmini ya utekelezaji wa sera iliyopita.

Ameiagiza ofisi ya rais tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI)kuhakikisha kuwa halmashauri zote nchini zinatenga asilimia 10 ipasavyo,halmashauri zitenge maeneo rasmi ya kuwawezesha wajasiriamali kuweza kujiajiri.

Kwa upande wake mkurugenzi mkuu kutoka mfuko wa kuendeleza huduma za fedha Tanzania (FSDT)SOSTHENES KEWE amesema asilimia 65 ya wananchi kwa sasa wanatumia  huduma za kifedha idadi ambayo imeongezeka tofauti na ilivyokuwa awali.

Serikali imekuwa ikifanya maboresho katika sekta ya fedha kuanzia miaka ya 1990 ili kukabiliana na changamoto katika sekta ya fedha na kuweka misingi imara yenye kukuza,ushindani na utendaji makini ambapo mwaka 2000 serikali iliandaa sera ya Taifa ya Huduma ndogo ya fedha.

LEAVE A REPLY